Uanahabari wa Upekuzi: Jinsi ya Kuielezea Sanaa Hii

Ijapokuwa maelezo ya uanahabari wa upekuzi hutofautiana, kuna makubaliano mapana miongoni mwa makundi ya kitaaluma ya uanahabari kuhusu nguzo zake muhimu: hufuata mfumo maalum, huwa na kina, hutegemea utafiti asilia na uandishi wa habari ambao mara nyingi huhusisha ufichuzi wa siri. Kwa wengine, upekuzi aghalabu huhusisha matumizi mengi ya data na rekodi za taarifa za umma, huku ukiangazia haki ya kijamii na uwajibikaji.

GIJN Africa: Ufadhili wa Kifedha

Uanahabari wa upekuzi siku zote umekuwa wenye gharama kubwa. Huku tasnia hii ikizidi kukumbwa na hali ngumu ya kiuchumi, mashirika mengi ya habari ya faida yamekoma kutengea upekuzi wa habari fedha nyingi kama ilivyokuwa hapo kabla.

GIJN Africa: Usalama na Ulinzi Barani Afrika

Katika asili yake yenyewe, uanahabari wa upekuzi ni tasnia yenye hatari ambayo huwaweka wanahabari na wahariri kwenye hatari mtandaoni na nje ya mtandao. Wanahabari wanaochimbua maasi ya maafisa wa serikali fisadi na maajenti wa ulinzi wakandamizaji hukabiliwa na vitisho vinavyolenga kuwakomesha au kudhibiti vyombo vya habari vyao hali kadhalika.

GIJN Africa: Kupata Rekodi za Umma

Katika mataifa mengi ya kusini mwa jangwa la Sahara, kupata habari za umma ni jinamizi mpaka leo. Hii ni kwa sababu hakuna sheria zinazofadhili maombi ya kupata rekodi za wanahabari, au zinazowashinikiza maafisa wa serikali kusalimisha rekodi za umma zinazomilikiwa na serikali.